Get The Marking Schemes Here
UFAHAMU (ALAMA 15)
Soma kifungu kifuatacho kasha ujibu maswali yanayofuata
Madhara ya sigara
Chimbuko la kuonekana kwa madhara ya tumbaku ilikuwa mwaka 1598 A.D. Madhara yake yaligundulika wakati ambapo makala ya kwanza ya kiafya iliandikwa nchini Uingereza ikieleza madhara ya sigara. Baada ya hapo zilifuatia tafiti mbalimbali zilizoendelea kugundua na kuelezea madhara yatokanayo na matumizi ya bidhaa za tumbaku kwa binadamu. Matokeo ya tafiti hizo yaliwezesha baadhi ya nchi kama vile Denmark, Uholanzi na Sweden kutunga sheria zinazozuia matumizi ya sigara. Katika sura ya pili, baadhi ya serikali zilikwazwa kiuchumi kwa kukosa pato la kodi zitokanazo na sigara na bidhaa zingine za tumbaku.
Mashirika na kampuni zinazojishughulisha na uzalishaji na uuzaji wa sigara hutenga fungu kubwa la fedha kwa ajili ya kutangaza bidhaa hiyo hatari kwa afya ya mwanadamu. Kila mwaka, Shirika la Afya Ulimwenguni hutenga siku maalumu ya kuelimisha jamii kuhusu athari za kiafya na madhara yatokanayo na matumizi ya tumbaku. Maadhimisho hayo hufanyika kila Mei 30 ya mwaka na kauli mbiu ya mwaka huu ilikuwa “Mkinge mwanamke kuwa mteja au kutumiwa kama mhamasishaji wa bidhaa zingine za tumbaku’.
Takwimu za shirika hilo zinabainisha kuwa asilimia 90 ya wavutaji sigara wameanzia umri wa miaka 18. Pia zimebainisha kuwa, kwa kila sekunde ipitayo, wastani wa mtu mmoja anafariki kutokana na madhara ya tumbaku. Inakadiriwa kuwa ifikapo mwaka 2025, vifo vitaongezeka kwa asilimia 70. Utafiti umebainisha ifikapo mwaka 2030, watu milioni 10 watakuwa wamefariki kutokana na kuvuta sigara.
Uvutaji sigara unasababisha magonjwa mengi kama vile saratani ya mapafu, wendawazimu, kupooza, matatizo ya mfumo wa hewa, kutoboka utumbo, kunyonyoka nywele, kupungua kwa nguvu za kiume, maradhi ya ngozi na kadhalika. Madhara ya tumbaku hayajitokezi mara moja. Huchukua kipindi kirefu hata miaka 30, hali inayowafanya wengi kufumbia macho tahadhari iliyopo, wakiendelea kuteketezwa na uvutaji sigara. Anayevuta sigara huathirika mapafu kutokana na moshi na tindikali – aina ya kaboni iliyomo kwenye tumbaku inayomzuia kupumua na mapafu yake huanza kutunga usaha. Hali hiyo huchangia mtu kupata athari nyinginezo kama vile kichomi, kifua kikuu na saratani. Chembechembe ya nikotini iliyomo katika tumbaku ni hatari kwa mvutaji kwani humpotezea mtu hamu ya kula na anapata maumivu makali ya tumbo.
Wakati wote, mvutaji sigara hutoa harufu mbaya mdomoni, hali ambayo haipendezi katika maisha ya mwanadamu, na pia, huwa anawadhuru wengine. Mtu huyo anapopumua huchafua mazingira kwa kupumua hewa chafu na mbaya zaidi ambayo huwadhuru watu walio karibu naye kama vile mwenza katika ndoa (mke au mume), watoto au marafiki.
Inaelezwa kuwa sigara huathiri akili ya mwanadamu kutokana na kuwepo kwa chembechembe za ulevi. Hali hiyo ipo zaidi mtu anapotumia sigara kwa mara ya kwanza kabisa. Utafiti wa kitaalamu umethibitisha watoto wanaolelewa katika mazingira ya wazazi wanaotumia sigara kuathirika mishipa inayosafirisha damu kwenda katika moyo. Hali hiyo husababisha kuharibika kwa mfumo wa usafirishaji damu mwilini kwa watoto hao na mwishowe wanakuwa wahanga wa maradhi tofautitofauti.
Katika sura ya pili ya kisaikolojia, watoto wanaokaa na wazazi wanaovuta sigara huishia kuifuata tabia hiyo na huo ndio huwa mwanzo wa kudhoofika kwa maadili. Kwa wajawazito, sigara ina madhara kama vile kuathiri ukuaji wa mimba na kondo la nyuma au placenta kwa Kiingereza na kushindwa kusafirisha chakula vizuri kutoka kwa mama kwenda kwa moto. Madhara mengine ni moto kuzaliwa na uzito pungufu, hivyo kuathiri ukuaji wake. Kwa hivyo, ni vyema kufahamu kuwa ingawa sigara ni bidhaa inayotumiwa kama uraibu wakati wa kuivuta, madhara yake ni janga kubwa linalopaswa kupigwa vita bila kuchoka.
Maswali
- Madhara ya sigara yalionekana mwaka gani ? (alama 1)
- Ni nchi gani zilizokuwa za kwanza kubuni sheria mpya kuhusu uvutaji wa sigara ? (alama 1)
- Uvutaji wa sigara una athari gani kwa anayevuta ? (alama 5)
- Watoto wanaathiriwa vipi na sigara ? (alama 4)
- Thibitisha kwamba uvutaji sigara hugharimu pesa nyingi. (alama 2)
- Eleza maana ya msamiati ufuatayo kama ulivyotumiwa katika kifungu. (alama 2)
- Kupooza
- Maadhimisho
LUGHA – SEHEMU B
- Kwa kuzingatia jinsi ya kutamka sauti za kswahili ni nini tofauti kati ya (alama 2)
- Irabu
- Konsonanti
- Eleza maana ya dhana hizi ( alama 2)
- Kiimbo
- Shadda
- Taja vipashio vine vya lugha (alama 4)
- Andika sentensi zifuatazo katika hali timilifu (alama 2)
- Mabati yananunuliwa
- Baba atakwenda dukani
- Kanusha sentensi zifuatazo (alama 3)
- Nchi za Afrika mashariki zalemewa na madeni.
- Mbu amemuuma mtoto.
- Baba ameandika barua ndefu.
- Zigeuze sentensi zifuatazo ziwe katika wakati uliopita (alama 2)
- Unapendelea kula nyama siku hizi.
- Opiyo alipenda kujiingiza katikati kama mchuzi wa ugali.
- Andika kwa wingi (alama 2)
(i)Maziwa ya mtoto yalimwagwa na paka yule.
(ii)Uvivu wa Juma unakera.
- Akifisha sentensi zifuatazo (alama 2)
(i)nenda sokoni ukaninunulie sukari maziwa na mkate
(ii)Maadam umeshafika tuanze mkutano
- Kamilisha jedwali lifuatalo kwa kuandika viambishi mwafaka kulingana na kitenzi (alama 5)
Kitenzi | Nafsi | Wakati | Kirejeshi | Kitendwa | Mzizi | kiishio |
Aliyelima Aliyempiga Anaoupanda Alipika Nitavileta |
- Taja vipera vya fasihi simulizi (alama 2)
- Onyesha vielezi katika sentensi zifuatazo (alama 2)
Mama amepika chai tamu sana
Nitakutembelea kesho jioni
- Nyambua vitenzi vifuatavyo katika kauli ya kutendwa (alama 4)
Piga –
Jenga –
Fagia –
Chora –
- Taja na ueleze dhima ya lugha (alama 2)
- Andika sentensi zifuatazo katika hali ya mazoea (alama 2)
- Mchoraji yule anachora picha nzuri
- Mpishi atapika chakula kitamu
- Bainisha maneno katika sentensi zifuatazo. (alama 4)
Salaala ! Majangili wamewaua ndovu kumi leo asubuhi
Wale watafungwa
FASIHI (ALAMA 15)
Taja majukumu matano ya fasihi ya kiswahili (alama 5)
Taja tofauti ya fasihi simulizi na fasihi andishi (alama 10)
ISIMU JAMII (ALAMA 10)
Nunua sabuni mpya ya GRESHA. It is new ! Harufu yake ni poa, inadumu siku yote, inalainisha ngozi. Ng’arisha nguo zako na sabuni ya GRESHA. GRESHA sabuni poa ! Bei yake ni nafuu; shilingi 20/= tu. Kila mtu ainunua.
Maswali
- Hii ni lugha gani ? (alama 2)
- Eleza sifa za lugha hii. (alama 8)
Insha (Aalama 20)
Andika insha itakayomalizikia kwa maneno haya ……………. “Nilipopokea mezani chakula kitamu nilikumbuka maisha magumu niliyoyapitia, nikatambua kuwa si rahisi kupata chakula kama hicho bila juhudi maishani.”