Find also Study Guide To ‘Bembea ya Maisha’-Mtiririko wa Maonyesho
Mwongozo wa Bembea ya Maisha’
UTANGULIZI
Mwongozo huu una nia ya kuwa mwanga gizani kwa wasomi wa diwani ya ‘Bembea ya Maisha’, kwa kutoa maelezo maridhawa kuhusiana na hadithi tofauti zilizomo humu. Ili kufanikisha hili, mwongozo huu umeangazia masuala kadhaa katika hadithi. Kabla ya kwenda katika hadithi binafsi, ni vyema kuangazia vipengele Fulani vya diwani.
MADA: Bembea ya Maisha.
1. ISTILAHI ZA LUGHA/ TAMATHALI ZA USEMI
Tashbihi/Tashbiha/Mshabaha. Hii ni mbinu ya kufananisha vitu viwili vyenye sifa sawa kwa kutumia vihusishi vya ulinganisho kama vile mithili ya, kama, sawasawa na, mfano wa na nyinginezo. Kwa mfano; Kamau ni mrefu mithili ya twiga.
Istiara/Sitiari. Hii ni mbinu ya kulinganisha vitu viwili vyenye sifa sawa moja kwa moja bila kutumia vihusishi vyovyote. Kwa mfano; Siku hizi amekuwa wali wa daku(yaani ameadimika, haonekani)
Tashihisi/Uhuishi/Uhaishaji. Ni mbinu ya kuvipa sifa za uhai vitu visivyo na uhai kama vile kuongea, kutangamana na kutekeleza mambo ya kibinadamu. Kwa mfano; hofu ilimkumbatia.
Methali. Ni tungo fupi zilizogawika katika sehemu mbili ambazo hubeba ujumbe wenye hekima. Huwa na maana ya juu, inayotokana na maneno yaliyotumiwa na maana ya ndani isiyohusiana na maneno hayo, ambayo huongoza matumizi yake. Kwa mfano; mla na miwili hana mwisho mwema.
Semi(Misemo na Nahau). Ni tungo fupi zinaoundwa kwa kuunganisha maneno, na ambazo maana yake na matumizi huwa tofauti na maneno yaliyotumika. Kwa mfano; enda segemnege- haribika, enda kombo.
Takriri/ Uradidi. Ni mbinu ya kurudiarudia neno au fungu la maneno kwa nia ya kutilia mkazo hoja fulani au kusisitiza. Uradidi huu unawea kutumiwa na mwandishi moja kwa moja katika usimulizi au ukatumiwa na mhusika katika mazungumzo. Kwa mfano;misitu kwa misitu ya mahindi na maharagwe.
Tabaini. Ni mbinu ya kutumia ukinzani kwa nia ya kudhihirisha wingi. Aghalabu hudhihirika kwa matumizi ya ‘si’ ya ukanushi. Kwa mfano; kila kitu kwake kilipendeza, si macho, si uso, si mavazi, si viatu, si sauti.
Chuku. Ni matumizi ya maelezo yaliyotiliwa chumvi kwa ajili ya kuonyesha uzito wa jambo au hoja fulani, na pia kumtumbuiza msomaji. Maelezo huelezwa kwa kiasi cha kuchekesha, kwani huzua hali ambazo ni wazi haziwezekani, lakini zinazokubalika kifasihi. Kwa mfano; hasira zake zingeweza kuivunja bilauri kwa kuiangalia tu.
Balagha/Maswali Balagha. Ni mbinu ya kutumia maswali yasiyohitaji majibu, kwa kuwa aidha majibu yako wazi, hayapo au hayahitajiki. Maswali haya husaidia kuelewa fikra za mhusika, kutoa taarifa zaidi au kumchochea msomaji kuwaza zaidi. Kwa mfano; kwa nini haya yanipate mimi?
Uzungumzi Nafsia/Monolojia. Ni mbinu ambapo mhusika hujizungumzia mwenyewe aidha kwa sauti au akilini. Huwezesha msomaji kujua mawazo, maoni au mipango ya mhusika. Kwa mfano;
“Muradi haya yashatokea, sina budi kukubali,” Mercy alijisemea moyoni.
Tanakali/ Tanakali za Sauti. Ni mbinu ya kuiga milio au sauti zinazotokea katika hali tofauti za kimazingira au sauti za wanyama na vitu tofauti. Kwa mfano; kriii! Kriii! Kriii! Simu yangu ilikiriza.
Dayolojia. Ni mbinu ya kutumia mawasiliano ya moja kwa moja kati ya wahusika wawili katika usemi halisi. Mawasiliano haya huhusu mada fulani wanayochangia wote. Mbinu hii busaidia kuonyesha mkinzano wa kimawazo, migogoro, maoni gofauti ya wahusika, n.k.
Kuchanganya Ndimi/ Lugha Mseto. Hii ni mbinu ya kutumia lugha mbili tofauti katika usemi, Kiswahili na lugha nyingine. Mara nyingi, maneno kutoka lugha ya pili huandikwa kwa mtindo wa italiki. Aghalabu huwa Kiingereza lakini yaweza kuwa lugha nyingine kama lugha ya mama,
Kiarabu, n.k. kwa mfano; “Mwanao ni mzima. He’s out of danger.”
Utohozi. Ni matumizi ya maneno kutoka lugha nyingine, aghalabu Kiingereza yaliyobadilishwa muundo na matamshi kuwa ya Kiswahili. Kwa mfano. Daktari(doctor), begi(bag), ticket(tiketi),n.k Kejeli/ Stihizai/ Dhihaka. Ni mbinu ya kutumia maneno ya kumsimanga mtu, tukio au suala fulani. Hali hii huweza kupunguza uzito wa hali au jambo au kumtilia mtu hamu ya kubadilika.
Inaweza kutumiwa na mwandishi mwenyewe katika maelezo ya suala au mhusika kwa mwingine.
Kwa mfano; alipata alama 10 katika hisabati. Kweli alijaribu, kama binadamu.
Nidaa. Ni mbinu ya kudhihirisha hisia za ndani kwa kutumia vihusishi na alama ya hisi(!). Kwa mfano, alifurahi sana kufika nyumbani. Popote ambapo alama hiyo imetumika, hiyo ni mbinu ya nidaa. Mtihani mkuu kwa mwanafunzi ni kufahamu hisia ambazo zinaakisiwa na alama hiyo.
Zinaweza kuwa furaha, huzuni, mshangao, mtamauko, hasira, amri, n.k. Laiti angalijua!
Koja. Ni mbinu ya kudhihirisha wingi wa vitu kwa matumizi ya koma kwa ajili ya kuorodhesha. Mbinu hii inaweza kuwasilisha kuwepo kwa lukuki ya vitu au mfuatano wa matukio mengi. Kwa mfano; Maria alifika nyumbani, akavua sare za shule, akaoga, akaenda mtoni kuchota maji, akapika, akala na kulala.
Mdokezo. Ni mbinu ya kuachia mambo yakining’inia, yaani kuacha bila kukamilisha ujumbe fulani kwa kutumia alama za dukuduku(…). Inaweza kuwa sehemu inayoweza kujazwa, itakayoelezwa mbeleni au kumwachia msomaji kujijazia. Pia inaweza kuwa zao la kukatizwa kalima wakati wa mazungumzo. Kwa mfano; aliingia ndani na kusubiri akijua wazi kuwa mgaagaa na upwa…
Tasfida. Ni mbinu ya kutumia msamiati wenye adabu ili kuepuka lugha chafu. Hutumika kuepuka lugha inayoweza kuzua hisia hasi au kutia kinyaa. Kwa mfano, mja mzito badala ya kuwa na mimba, kubaua/kutabawali au kwenda haja ndogo badala ya kukojoa.
Tadmini. Ni mbinu ya kutoa marejeleo katika misahafu(vitabu vya kidini) kama vile Biblia na Korani, na kuyahusisha na hali fulani katika kazi ya kifasihi. Kwa mfano; ukaidi haujaanza leo, ulianza na Adamu na Hawa kwenye bustani la Edeni.
Tanakuzi. Ni mbinu ya kutumia maneno yenye kinyume katika sentensi moja na kuzua kauli zenye ukinzani. Aghalabu hutumika kuonyesha hali ya utata. Kwa mfano; asali iligeuka shubiri. Alikufa na kufufuka ilipobidi.
Lahaja. Ni matumizi ya maneno ya lahaja tofauti za Kiswahili ambayo hayapo katika Kiswahili sanifu. Upekee wake ni matumizi ya maneno yasiyo ya Kiswahili sanifu bali vilugha vyake. Kwa mfano; kahawa tungu(kahawa chungu), mwananti kuivunda nti(mwananchi kuivunja nchi).
Mwongozo wa Bembea ya Maisha’
2. MBINU ZA KIMTINDO
Sadfa. Ni mtindo ambapo matukio mawili yanayohusiana hutukia kibahati kwa wakati mmoja, au kwa mfululizo kama kwamba yamepangwa. Matukio haya aghalabu huwa na matokeo fulani. Kwa mfano; kukutana na msaada wakati wa tatizo bila kutarajia.
Kinaya. Ni mtindo ambapo matukio huenda kinyume na matarajio yetu, aidha kulingana na mfululizo wa awali wa matukio, au kwa kuyalinganisha na maisha halisi. Pia mbinu hii inaweza kudhihirishwa kupitia kwa usemi wa mhusika. Kwa mfano; kumpa hongera mtu aliyefeli au kusherehekea baada ya kufeli.
Majazi. Ni mtindo wa kuwapa wahusika majina kulingana na tabia au maumbile yao. Majina haya huitwa majina ya majazi/kimajazi. Kwa mfano; mtu katili anaweza kupatiwa jina ‘Kedi’.
Taswira. Mtindo wa kutoa maelezo ya ndani kuhusu suala fulani kiasi cha kujenga picha ya kile kinachorejelewa kwenye akili ya msomaji. Kuna taswira toofauti kama vile mwonekano, mnuso au harufu, hisi na mguso, kulingana na picha inayozalishwa. Kwa mfano; kaptura yake nyeusi iliyochakaa ilirembwa kwa viraka vya kila rangi, hungetambua rangi yake asilia.
Taharuki. Ni mtindo wa kutoa maelezo taratibu kwa kusaza habari fulani ili kumtia msomaji hamu ya kujua zaidi. Pia huweza kumwacha msomaji akining’inia mwishoni mwa kisa na kumwacha kujijazia kuhusu masuala fulani.
Kisengerenyuma/Mbinu Rejeshi. Ni mtindo wa kurejelea matukio yaliyotukia muda uliopita, lakini yenye uhusiano na yale yanayosimuliwa. Yanaweza kurejeshwa na msimulizi au mhusika fulani kupitia kumbukumbu zake.
Kiangaza Mbele/Kisengerembele/Kionambele. Ni mtindo wa kudokeza mambo yatayotukia mbele kabla hayajatukia, na kuyahusisha na yale yanayotukia wakati huo.
Utabiri. Ni mbinu ambapo mhusika hudokeza jambo kisha likatukia baadaye bila yeye kutarajia. Tofauti yake na Kiangazambele ni kwamba utabiri huwa jambo la kukisia au kudokeza tu, bila uhakika wake wa kutokea.
Jazanda. Ni ufananisho wa mzito wa vitu viwili visivyo na uhusiano wa moja kwa moja, ambavyo hulinganishwa na kulinganuliwa kwa njia ya mafumbo. Kwa mfano, Bi. Sarafu alilalamika kuwa jembe la mumewe lilishindwa na kazi.
Ishara. Ni mambo, vitu au matukio ambayo huonekana au kutukia kabla ya jambo fulani yanayoashiria. Mambo haya huwa na uhusiano fulani na matukio yanayoashiria. Kwa mfano; milio ya bundi inayomtia mhusika wasiwasi kabla ya janga fulani kutokea.
Ritifaa. Ni mtindo ambapo mhusika aliye hai humzungumzia mhusika aliyefariki kama kwamba yuko hai na anamsikia. Huweza kuonyesha uhusiano kati yao, kueleza hisia za ukiwa au kumtakia neema.
Lakabu. Ni matumizi ya majina ya kupanga kuwarejelea wahusika. Majina haya huambatana na sifa fulani za mhusika. Tofauti na majazi ni kuwa lakabu huwa majina ya kupanga, bali si majina halisi ya wahusika.
Mwongozo wa Bembea ya Maisha’
Ushairi Nyimbo. Barua
Mwingiliano wa Vipengele.
Ni muhimu kuelewa kwamba kuna mwingiliano wa kipekee katika vipengele hivi tofauti vya hadithi, kwani haviwezi kushughulikiwa kwa ukamilifu. Baadhi ya mwingiliano ni kama ufuatao;
Dhamira ya Mwandishi na Maudhui. Dhamira ndiyo huongoza maudhui ambayo yanashughulikiwa katika hadithi. Hivyo basi, mambo haya mawili huingiliana pakubwa. Dhamira ndiyo hufungua nafasi kwa maudhui ya hadithi. Kwa mfano, iwapo mwandishi anadhamiria kudhihirisha maovu yanayotendewa wananchi na wanasiasa au viongozi, lazima kuwepo maudhui ya siasa au uongozi au yote.
Dhamira na Wahusika. Kila dhamira huwasilishwa kwa kutumia mhusika au wahusika fulani. Bila wahusika, dhamira haiwezi kutimizwa wala wahusika hawawezi kuwa na maana bila dhamira. Sifa za wahusika zinalingana na dhamira na kubwa zaidi, umuhimu wao huhusiana moja kwa moja na dhamira ambayo wanatekeleza. Kwa mfano, iwapo mwandishi anadhamiria kudhihirisha madhila ya wanawake katika jamii, lazima awepo mwanamke anayetekeleza dhima hiyo.
UTANGULIZI
VIGEZO MUHIMU KATIKA UCHAMBUZI WA TAMTHILIA HII
- Dhamira/ Lengo/ Mintarafu/ Kusudi: Nijambo linalokusudiwa na mwandishi/ lengo kuu la mwandishi.
- Maudhui: Jumla ya maswala yanayozungumziwa na mwandishi 3) Falsafa: Msimamo wa mwandishi kuhusu jambo fulani analoliandikia.
- Muwala: Mtiririko wa vitushi/ mawazo katika kazi ya fasihi.
- Usuli: Asili /hali inayomzunguka mwandishi na ambayo humchochea kuandika kazi ya fasihi
k.m. usuli wa mwandishi waweza kuwa anazungukwa na jamii iliyojaa uongozi mbaya / ufisadi ndiyo maana anaandika kuhusu maudhui hayo.
- Mandhari: Mahali ambapo wahusika wanatekelezea kazi ya fasihi. K.m. njiani, shuleni n.k.
- Wahusika: Ni viumbe ambao huendeleza mawazo ya mwandishi katika kazi ya fasihi. Wahusika waweza kuwa binadamu, Wanyama, viumbe halisi au wa kidhahania (wa kufikirika tu).
AINA ZA WAHUSIKA KATIKA FASIHI
1) Wahusika wakuu
- Huchukua nafasi kuu na kukuza kazi ya fasihi.
- Matendo yote muhimu huwahusu.
- Dhamira kuu ya mwandishi na falsafa/ msimamo wake hudhihirika kupitia kwa wahusika wakuu.
2) Wahusika wadogo
- Hawana nafasi kubwa.
- Aghalabu husaidia hadhira kujua zaidi mhusika mkuu na dhamira yake.
3) Wahusika wasaidizi
- Hujenga wahusika wakuu na kukuza maudhui. Aghalabu huja na kutoweka baada ya muda mfupi.
- Uainishaji Mwingine wa Wahusika
4) Wahusika bapa/ Wahusika wa mraba mmoja
- Huwa hawabadiliki katika hulka/ sifa zao.
- Mhusika bapa anaweza kuwa na tabia nzuri au hasi kuanzia mwanzo hadi mwisho.
5) Wahusika duara/ wahusika wa miraba minne
- Huweza kubadilika kisaikolojia.
- Huwa na sifa nyingi.
- Wahusika bapa vielelezo
- Huwa na tabia za kubadilika ila hujikita katika mtazamo wa mwandishi na hadhira yake.
- Aghalabu huwa wahusika wakuu na hutumiwa na mwandishi kuendeleza suala fulani.
6) Wahusika bapa sugu
• Wana sifa ya kutobadilika ila huwakilisha walio na tabia potovu katika jamii. Mhusika bapa sugu anayeweza kuwa mhusika mkuu.
7) Wahusika hasidi/ wapinzani
- Hulka zao ni kinyume na mtazamo wa maadili ya jamii.
- Humpinga mhusika nguli.
8) Mhusika nguli
• Ni mhusika anayekinzana na mhusika hasidi kwani anawasilisha maadili katika kazi ya fasihi.
Aghalabu huwa mhusika mkuu au mmoja wa wahusika wakuu.
Mwongozo wa Bembea ya Maisha’
9) Mhusika shinda
- Hukuza wahusika wengine kwa kuwa hupelekwa mbele kwa usaidizi wa wahusika wengine.
- Huwa chini ya kivuli cha mhusika mkuu.
- Kupitia kvake ndipo hadhira inapata sifa bayana za wahusika wakuu.
FANI ZA FASIHI/ MITINDO KATIKA FASIHI
Fani ni mbinu ambazo hutumiwa na mwandishi anapoiandika kazi ya fasihi.
Fani hujumuisha:
- Mitindo ya lugha: Pia huitwa matumizi ya lugha, mitindo ya lugha, tamathali za lugha, mbinu za
lugha au tamathali za usemi.
- Mintindo ya uandishi: Pia huitwa fani za mwandishi, mbinu za uandishi, mbinu za sanaa au mbinu za usanii.
FANI ZA LUGHA (TAMATHALI ZA USEMI)
Ni maneno, sentensi au misemo inayotumiwa kuwasilisha kazi ya fasihi. (Senkoro; 1982).
Zinajumuisha:
- Takriri/ Uradidi (Repetition): Takriri ni mbinu ya lugha ambayo kwayo maneno au silabi fulani hurudiwa. Lengo kuu la takriri huwa ni kusisitiza jambo fulani na kuwavutia wasomaji wawazie jambo hilo.
- Maswali Balagha/ Mubalagha (Rhetoric; questions): Haya ni maswali ambayo hayahitaji majibu. Jibu la swali la balagha huwa akilini mwa anayeulizwa au anayesoma kazi fulani ya fasihi au huwa tayari analijua. Dhima ya maswali balagha huwa kutoa mawazo au hisia za ndani za mhusika au kuweka jambo fulani wazi. Aidha hulenga kusisitiza usemi fulani na kuwasilisha maudhui.
- Methali: Ni kauli fupi ya kimapokeo inayosheheni maana na ujumbe na ambayo huwa na mizizi katika jamii. Methali huwa na wingi wa hekima na hutumiwa kupigia mfano. Huwa na maana iliyofumbwa.
- Tanakali ya sauti: Ni mbinu ambapo mwandishi huiga tendo fulani na kulipa matamshi au maandishi.
- Tashbihi/ Tashbiha/ Mshabaha: Ni ulinganishi/ umithilishaji (usio wa moja kwa moja) wa kitu na kingine kwa kutumia maneno kama vile: ja, mfano wa, mithili ya, kama, sawasawa, ungedhani ni… .n.k.
- Istiara/ Sitiari: Ni ulinganisho wa kitu na kingine kwa njia ya moja kwa mojae Ulinganishi huu hufanywa bila kutumia vifananishi.
- Nidaa: Ni maneno ambayo hutumiwa kuonyesha hisia za wahusika. Hutumika kuonyesha hisia za furaha, huzuni, masikitiko, mshangao, mshtuko n.k.
- Jazanda: Mwandishi hutaja kitu fulani ambacho kwa kawaida kinaweza kuonekana kuwa na maana ya kawaida ila kinapochunguzwa zaidi kinaonekana kuwa na maana ya ndani kuliko ile ya kawaida. Jazanda ni sawa na kilichositiriwa ndani mwa neno au maneno fulani.
- Mdokezo: Mbinu ambapo mhusika mmoja hutaja jambo kisha mwenzake hulikamilisha au mhusika hutoa wazo/ jambo na kumwacha msomaji kulikamilisha. Aidha, mdokezo waweza kutokea palipo na upinzani ambapo mhusika mmoja anaweza akatoa jambo huku mwenzake akilikamilisha atakavyo kwa kumpinga au kumkejeli.
10)Tabaini: Tabaini ni mbinu ya lugha ambapo mwandishi hutumia maneno kueleza jambo linaloeleweka waziwazi na msomaji. Ni maelezo ya kina kuhusu j ambo. Waandishi wengi hutumia takriri/ neno moja ili kuibua tabaini. K.m. urudiaji wa ‘ni’ na ‘si’. K.v. Walifika watu wa janibu mbalimbali: si wanawake, si wanaume, si vijana, si watoto — wote walijumuika kumuaga gwiji wa taarabu.
11)Taniaba: Taniaba yatokana na ‘kwa niaba ya’. Kitu/ Jambo hutumiwa kuwakilisha au kufanya kwa niaba ya kitu/ jambo jingine. K.m. chaki ni taniaba ya mwalimu; jembe ni taniaba ya mkulima ilhali bunduki ni taniaba ya askari.
12)Utohozi: Ni mbinu ya kuswahilisha maneno ya lugha nyingine ili yatumike kama ya Kiswahili. K.m. skwota — Squatter, ekisirei X-ray n.k.
13)Tasfida/ Tauria/ usafidi (Euphemism): Matumizi ya lugha ya adabu/ ya sitara/ ya nidhamu. K.m. Natoka kutabawali (Haja ndogo) badala ya natoka kukojoa; Alijifungua badala ya alizaa n.k.
14)Chuku/ Udamisi (Exaggeration/ Hyperbole): Mbinu ya kuongeza chumvi katika jambo. Mwandishi hueleza jambo kwa namna inayozidi hali halisi ya jambo hili. K.m. watu waliohudhuria matanga walikuwa wamcjaa pomoni hivi kwamba hapakuwa na nafasi ya nzi kupita.
15)Ucheshi/ Kichekesho (Humour): Maneno yanayozua furaha. Msomaji hucheka kutokana na namna mwandishi alivyolieleza jambo.
16)Kejeli: Pia huitwa dhihaka, kebehi, stihizai au mcheko. Ni kumfanyia mtu, jambo au kitu dhihaka au kumdunisha mtu au kitu kwa kuonyesha kuwa anachosema hakina thamani.
17)Lakabu: Mbinu ya mhusika kupewa au kubandikwa jina na wahusika wengine au yeye mwenyewe kujibandika jina linaloambatana na sifa zake.
18)Kuchanganya ndimi (Code mixing): Pia inaitwa kuchanganya lugha, kuchanganya msimbo au ndimi mseto. Ni mbinu ya kuweka maneno yasiyo ya Kiswahili katika sentensi ya Kiswahili. K.m.
Sina time ya wanawake.
19)Kubadili msimbo (Code switching): Pia huitwa kuhamisha msimbo, kuhamisha ndimi au kuhamisha lugha. Ni mbinu ya kuchopeka sentensi ya lugha nyingine katika kifungu cha lugha ya Kiswahili. Utofauti kati ya kuchanganya ndimi na kubadili ndimi ni kuwa katika kuchanganya ndimi, mwandishi huchanganya maneno ya Kiswahili na lugha nyingine katika sentensi moja ila katika kubadili ndimi, sentensi kamilifu ya lugha nyingine hutumika miongoni mwa sentensi sanifu za Kiswahili.
20)Ritifaa: Ni mbinu ya kuzungumza na mtu asiyekuwepo au aliyekufa. K.m. Mbona umeamua kuniacha duniani?
21)Taashira (Symbolism): Ni mbinu ya kutumia lugha ya ishara kuwakilisha ujumbe fulani.
22)Majazi: Mwandishi huwapa wahusika majina yanayoambatana na tabia au hulka zao.
FANI ZA UANDISHI (MBINU ZA SANAA)
- Taharuki (Suspense): Ni mbinu ya kumpa msomaji hamu/ tamaa ya kuendelea kusoma ili kujua kitakachofanyika baadaye.
- Sadfa (Coincidence): Matukio mawili hutokea kwa wakati mmoja bila kutarajiwa, kupangwa au kukusudiwa.
- Barua/ Waraka: Wahusika huandikiana barua. Nyimbo na Mashairi d) Ndoto/ Njozi/ Ruiya:
Maono ya mhusika akiwa amelala.
- Uzungumzi nafsia/ Mjadala nafsia: Mhusika hujizungumzia mwenyewe.
- Mbinu rejeshi/ Kisengere nyuma: Mwandishi hurejelea mawazo ya msomaji kwa matukio ya awali hasa kupitia kwa masimulizi.
- Kinaya: matukio katika kazi ya fasihi kuwa kinyume na matarajio ya msomaji au hali halisi.
- Usemaji kando: Mhusika anayezungumza na wenzake hutafuta faragha labda kwa kuzungumza bila kumhusisha mwenzake au kupinda kichwa. Mhusika mmoja anaweza kuwa anamsengenya mwenzake/ au anapinga maoni ya mhusika mwenzake.
- Tadmini: mbinu ya kuchukua mtindo wa lugha au maneno kutoka kwa matini nyingine na kuweka katika matini fulani. Kwa mfano kuchukua vifungu vya Biblia kutoka matini ya Biblia na kuyatumia katika tamthilia. K.m. Amini amini nakwambia. (Kigogo).
- Hotuba: mazungumzo ambayo hutolewa kwa hadhira na mtu mmoja. Mazungumzo haya
aghalabu huhusu jambo maalum.
- Tashihisi: pia huitwa uhuishi, uhaishaji au uhuishaji. (Personification): Ni mbinu ya kuvipa vitu visivyo na uhai sifa za au kutenda kama kitu kilicho na uhai.
- Utabiri/ ubashiri: Ni mbinu ya kueleza kuhusu mambo ambayo yatatokea baadaye.
- Mhusika ndani ya mhusika: mhusika fulani huiga maneno au matendo ya mhusika mwingine
na kutenda kama yeye.
- Mbinu maarifa mtambuka: Msanii kuingiza maarifa ya taaluma (uwanja mwingine wa
kitaaluma) katika kazi yake.
- Taswira: Ni mbinu ya mwandishi kutoa maelelzo kuhusu jambo au mtu yanayojenga picha (Mawazo ya akilini) ya jambo au mtu huyo hivi kwamba msomaji huona picha kamili ya kitu/ jambo au mahali hapo. Dhima ya taswira huwa kumwezesha msomaji aelewe zaidi jambo husika.
AINA ZA TASWIRA
- Taswira muonjo/ mwonjo: msanii anaweza kutueleza namna chakula kilionjwa hadi msomaji
akataka adondokwe na mate.
- Taswira oni: msanii hutoa maelezo hadi msomaji akaona picha ya kitu/ jambo fulani mawazoni. iii) Taswira hisishi: msanii anaweza kueleza hisia za mhusika fulani kama furaha, majonzi n.k.
iv) Taswira msanii anaeleza jinsi ambavyo alisikia jambofulani kwa nakini. v) Taswira mnuso:
msanii anaeleza mambo kuhusu harufu anayoingiamua kupitia pua,
vi) Taswira mguso; msanii anaeleza alivyohisi kwa mguso.
Katika maandalizi ya kuukabili mtihani(kuyajibu maswali), ni vyema mwanfunzi azingatie mambo yaliyo hapa chini ili aweze kuyamudu maswali yatakayotokana na kazi anazozishughulikia.
Isome kazi mara kadhaa ili kuifahamu kazi husika ndani nje. Kuisoma kazi mara moja na kujidanganya kuwa umeielewa si vyema. Hakikisha kuwa umeyafahamu mambo yote muhimu katika kazi ya fasihi na kuyahifadhi katika ncha za kucha zako(yakumbuke kwa urahisi).
Wakati wa kusoma kazi hizi, hakikisha kuwa una penseli ili kupiga nmstari mambo yote muhimu
k.m mbinu za lugha, wahusika, nk. Vile vile hakikisha unaongeza pembeni mambo yote muhimu yanayojitokeza unapoendelea kutagusana na kazi.
Fahamu kuwa sehemu hizi tatu hutahiniwa. Kila sehemu hubeba alama 20. Wakati wa kuyajibu maswali ya mtihani, mwanafunzi achague maswali ambayo anayamudu vilivyo ili kujizolea alama nyingi zaidi.
Mwanafunzi vilevile asipuuze mambo mawili yafuatayo wakati wa kuukabili mtihani;
HATI
Hati ni mwandiko yaani namna mtu anavyoandika. Hati huwa kigezo muhimu sana katika mtihani.
Ni vyema mwanafunzi aandike kwa hati inayosomeka vyema kwa urahisi. Ukiandika kwa hati ‘nadhifu’ mtahini hatatatizika kuisoma kazi yako wala kutumia muda mwingi akijaribu kuisoma kazi yako. Ni vyema uzingatie namna ulivyofundishwa kuandika herufi katika chekechea. Herufi zingine zisizoeleweka ambazo wanafunzi huweza kuandika si za Kiswahili na hazina maana katika Kiswahili, ziepuke.
Makosa ya kisarufi
Japo makosa haya hayaadhibiwi katika karatasi hii ya 102/3, ni vyema mwanafunzi ayaepuke mno. Makosa haya yakikithiri yanaweza kuupotosha usahihi wa jibu kiasi cha mtahini kuamua kukuadhibu na bila shaka utakuwa umepoteza alama. Makosa mengine ya kuingiza herufi zisizo za Kiswahili kama vile ‘X’, ‘C’ nek katika kuendeleza maneno ya Kiswahili visivyo pia hupotosha umantiki na usahihi wa jawabu.
Mwongozo wa Bembea ya Maisha’
JINSI YA KUKABILIANA NA MASWALI
Baada ya kuisoma kazi yoyote ile ya Fasihi Andishi, mtihani hufuata. Kwa hivyo ni vyema kujihama na mbinu za kuyakabili maswali.
Mwanzo, fanya utafiti zaidi kuhusu usuli wa kazi unayasoma, falsafa au mtazamo wa mwandishi
n.k. Ihakiki kazi yenyewe kwa undani ili kuhakikisha umeelewa maudhui, wahusika, matumizi ya lugha, mandhari na fani nyingine zilizomo. Ili kujitayarisha kuyajibu maswali katika mtihani wa fasihi, ni muhimu kuelewa kuhusu Uteuzi wa maswali.
Tatizo kubwa linalowakumba watahiniwa katika mtihani wa fasihi ni uteuzi wa maswali. Kati ya maswali saba yanayotahiniwa, mtahiniwa anatakiwa kuchagua maswali manne.
Ikumbukwe kuwa Riwaya, Tamthilia na Hadithi Fupi ni kati ya maswali haya saba yaliyotahiniwa.
Kwa hivyo, hakikisha unaangazia yafuatayo katika sehemu hii;
- Uzito wa swali – kadiria uzito wa maswali kwa kuangalia alama zinazotolewa kando ya swali.
Swali la alama 20 linahitaji hoja kumi zilizojadiliwa vyema.
- Hoja za kutosha. Usivamie maswali bila kuwa na hakika kama una hoja za kutosha kuyajibu kwani huenda utakwama katikati. Kama swali lina alama 20, hakikisha una hoja kumi zenye uzito.
- Kulielewa swali – Elewa swali na kuangalia kama lina vijisehemu. Iwapovijisehemuvyake
vinahusiana na sehemu ya kwanza, jihadhari usije ukakosa kuonyesha uhusiano huo. chukua muda kuchagua swali, kwa
- Kuchagua swali kuandika vidokezo vya kulijibia kando ya swali lenyewe. Ni vyema kuchagua swali ambalo utapata zaidi ya alama 15.
- Kuyaelewa maagizo kumbuka kuwa, maswali hutungwa ili kujibiwa kwa kuzingatia maagizo. Unapaswa kulichukua jukumu la kusoma, kuelewa na kufuata maagizo. Kwa mfano, kuna maswali ambayo ni ya lazima, na maswali ya kuchagua. Kadhalika, maagizo hufafanua jinsi ya kuchagua maswali, k.v. jibu swali la tatu au la nne. Usijibu maswali mawili kutoka kitabu kimoja na kadhalika.
- Kuuelewa msamiati wa swali — pamoja na maagizo, zingatia pia msamiati wa swali. Kwa
mfano unapoambiwa – taja na ueleze, lazima uelewe kwamba, mtahini katika mwongozo wake wa kusahihisha, atakuwa na tuzo yakutaja mambo manne, kwa mfano, aghalabu utakuta neno manne limekolezwa wino.
Hakikisha kuwa una hoja nne zilizo sahihi. Iwapo utaandika hoja zaidi ya nne, mtahini atachukua hoja nne za mwanzo tu, hata kama umezikosea na hatatuza hoja zinazofuata japo zitakuwa sahihi.
AINA ZA MASWALI
Kuna aina mbalimbali za maswali. Kila moja yazo huwa na mahitaji yake. Kuna aina mbili za maswali yanayotokea katika tamthilia na vitabu vingine viteule: maswali ya insha na maswali ya muktadha wa dondoo.
Maswali ya insha huandikwa kwa nathari. Jiepushe na kudondoa hoja au kuziorodhesha. Wakati ambapo maswali ya insha yanahitaji majibu ya kina na hoja zilizofafanuliwa kikamilifu, yale ya muktadha yanamhitaji mtahiniwa awe ameielewa tamthilia kwa undani ili aweze kufafanua muktadha wa dondoo alilopewa bila kukatizika. Hii itamwezesha kulitambua dondoo lilikotolewa kwa urahisi.
Katika kufafanua muktadha wa dondoo, mtahiniwa anahitajika kujibu maswali manne kwa usahihi:
- Nani anaongea?
- Anaongea aongea na nani?
- Wakiwa wapi au katika hali gani?
- wanaongea kuhusu jambo gani?
JALADA LA BEMBEA YA MAISHA
Jalada ni sehemu iliyoko juu ya kitabu Huwa ni mambo yaliyo muhtasari wa kile msomaji anataraji ndani. Jalada huwa kuwili yaani, jalada la mbele na la nyuma. Kunavyo vipengele muhimu hasa rangi za michoro na maandishi.
Jalada la tamthilia ya Bembea ya Maisha limechorwa mwanamume na wanawake wawili wakiwa wamekumbatiana. Watu hao wameketi kwenye bembea. Mwanamume huyo anawakilisha Yona na wanawake hao wanawakilisha Sara na Neema.
Wote wanaonekana kufunga macho kuonyesha wako katika hali ya utulivu wa moyo. Hali hii ya kukumbatiana inadhihirisha kwamba kuna upatanisho wa familia ambayo ilikuwa imeyumbishwa na bembea ya maisha.
ANWANI YA TAMTHILIA
- Bembea ni kifaa kama vile ubao, kamba au chuma inayoninWinia baina ya chuma au mti ambacho hutumiwa kuchezea aghalabu na watoto.
- Bembea huenda juu na chini au mbele na nyuma. Ili mtoto aweze kucheza na bembea, wakati mwingine kuna anayeisukuma bembea hiyo.
- Bembea ya maisha ni namna maisha yanavyoendesha watu.
- Katika tamthilia hii, maisha yamesawiriwa kama bembea. Kuna wakati maisha ya wahusika yamejawa na furaha na mafanikio tele na kuna wakati maisha ya wahusika yanaenda chini, wanakumbwa na shida na matatizo.
Kwa mfano:
Maisha ya familia ya Sara na Yona yanaleta taswira ya bembea. Mwanzoni, ndoa ya Sara na Yona inaonekana yenye furaha. Hii ina maana kuwa, kama bembea inavyokuwa juu, maisha yao yalikuwa yenye mafanikio na furaha. Maisha yao yanaingiwa na dosari wakati wawili hao wanakosa mtoto baada ya kipindi kirefu katika ndoa. Zaidi ya hayo, wanajaliwa na watoto wa kike watatu. Hawajaliwi na mtoto wa kiume, kinyume na matarajio ya jamii. Wanachekwa, wanasutwa na kukejeliwa.
Bembea ya maisha yao inarudi chini. Sara anaanza kuchapwa kichapo cha mbwa na bwana yake
Yona. Yona anaidharau familia yake na kuingilia ulevi, ulevi uliomfanya kupigwa kalamu kazini. Sara anasema, japo kuna wakati maisha yanabwagwa na bembea ya maisha, lazima maisha hayo yaendelee. Hata kama kamba, chuma au minyororo ya maisha inakatika, hawana budi kujiinua na kuendelea na maisha (uk. 20-21). Hivyo basi Sara anasimama na familia yake kidete akifahamu kuna siku atafanikiwa na maisha yao yatakuwa mema tena.
Maisha ya familia ya Yona yanabadilika kutoka kuwa maisha ya kukosa mahitaji ya kiuchumi. Bembea yao ya maisha ilionekana kuwachini. Baada ya Neema kufanikiwa na kupata kazi, bembea ya maisha yao inakuwa juu. Wanafanikiwa kujengewa nyumba, wanapata wafanyakazi wa kuwasaidia nyumbani na hata kuwa na jiko la gesi la kupikia.
Bembea ya maisha ya Neema inaonekana kusukumwa na Bunju mumewe. Kwanza Bunju alimsaidia Neema alipokuwa amepata ajali. Bunju alimtumia flying doctors ili aweze kupata matibabu zaidi (uk. 41).
Bunju anasaidia kuisukuma bembea ya maisha ya Neema kwa kumsaidia kuwasomesha dada zake.
Vilevile, anamsaidia kuwajengea wazazi wa Neema nyumba.
Maradhi ya Sara yanaifanya bembea ya maisha ya Sara kuwa kama iliyokatika na kuwa chini. Sara anakosa matumaini ya kuishi na kutamani kufa.
Bembea ya maisha ya mjini huwa juu kutokana na maendeleo. Kuna maendeleo ya barabara, magari mengi, majengo mengi na hata sekta ya matibabu imeimarishwa.
Watu mjini wanapokea matibabu ya hali ya juu ilhali, bembea ya maisha ya kijijini huwa chini kwa sababu ya kukosa maendeleo hasa katika sekta ya matibabu na barabara nzuri. Sekta ya matibabu ya kijijini inamfanya Neema kumtafutia mamake hospitali ya mjini sababu zile za kijijini hazimpi mtu matumaini ya kutoka akiwa mzima ilhali za mjini zinampa mgonjwa matumaini ya kutoka akiwa buheri wa afya.
Mwongozo wa Bembea ya Maisha’
Dhamira ya mwandishi
Dhamira huelezwa kama lengo au shabaha ya mwandishi wa kazi ya fasihi. Mwandishi wa tamthilia ya Bembea ya Maisha anadhamiria:
🙓 kuonyesha masaibu ya pombe katika maisha ya familia
🙓 kuonyesha kuwa ili kujenga jamii mpya, mapinduzi ni muhimu na ni lazima wanajamii wajitolee kupinga tamaduni zisizo na umuhimu wowote katika maisha ya wanajamii
🙓 kutuonyesha kuwa watoto wa jinsia zote ni sawa na hawafai
🙓 kutenganishwa kwa mila na tamaduni za jamii
🙓 kutuonyesha kuwa hakuna lililo na mwanzo lisilokuwa na mwisho.
1 thought on “Study Guide To ‘Bembea ya Maisha’by John W. Wanjala-Part 1”