KCSE Predictions Ushairi Questions And Answers- Shairi 6-10
USHAIRI WA 1
Soma shairi lifuatalo kwa makini halafu ujibu maswali yanayofuata
- Naja sasa ni ndiyani, naja kwetu Mzalendo
Naja nirudi nyumbani, nilowekwa nako kando
Kwetu’ mi nakutamani, kulo na mwingi uhondo
Nijaye ni yule nyundo, misumari hadharini
- Naja kwingine kuwapi, kulojaa langu pendo?
Huenda nende kwinginepi, sawa nako kwa muundo?
Kaa kwingine anapi, ela kwenye lakwe gando?
Nijaye ni ile nyundo, misumari hadharini
- Naja nije rudi papo, panigedeme mgando
Ningaambwa kwetu hapo, kwamba kwanuka uvundo
Sitakwenda penginepo, tarudi kuko kwa mwando
Nijaye ni ile nyundo, misumari hadharini
- Naja sitapakimbiya, ningambwa kuna vimondo
‘Takuja kuvilekeya, vinganijiya kwa vundo
nilipozawa tafiya, sikimbii kwenda kando
nijaye ni ile nyundo, misumari hadharini
- Naja hiwa ‘mekomaa, kuzidi nilivyo mwando
Tena n’najiandaa, kwa fikira na vitendo
Kwetu nije kuifaa, na kuitiliya pondo
Nijaye ni ile nyundo, misumari hadharini
- Naja na ingawa naja, siwaeki mifundo
Moyo wangu ushatuja, mawi nalotendwa mwando
Ela wataoningoja, na vyao viwi vitendo
Nijaye ni ile nyundo, misumari hadharini
7. a) Eleza jinsi ‘uzalendo’ wa mshairi unavyojitokeza katika beti za 1 na 2 alama 4
- Fafanua jazanda zinazopatikana katika mshororo:
Kaa kwingine anapi, ela kwenye lakwe gando? alama 2
- Andika ubeti wa tatu katika lugha nathari alama 4
- (i) Katika ubeti wa 5 mshairi amebadilika Eleza alama 2
(ii) Ananuia kufanya nini pindi arudipo? Alama 2
- Eleza ujumbe unaopatikana katika ubeti wa 6 alama 2
- Andika maneno haya katika kiswahili sanifu alama 2
- Mwando
- Ningambwa
- Kibwagizo cha shairi kinampa sifa gani mshairi? Alama 2
MWONGOZO WA KUSAHIHISHA SHAIRI WA 1
7) `UZalendo’
(i) Anarudi kwao
(ii) Anapenda kwao
(iii)Anatamani kwao
(iv) Nyumbani kunamlisha
(v) Ndiko kuna uhondo
(vi) Hawezi kulinganisha kwao na kwingine zozote 4 x 1 4
b) Jazanda
(i) Anajilinganisha na kaa na angeishi baharini mahali pakubwa
(ii)Kaa ana lile gando, kile kifaa anachokitumia kupatia chakula na vile vile kama silabi, paini nyumba ambapo pana chakula na usalama au mtu kwao ni kwao ndipo pampapo riziki/ ussalama na utulivu
2×1 = 2
c) Lugha Nathari
(i) Ninarudi hapo kwetu
(ii) Hata nikiambiwa pananuka
(iii) Siendi pengine narudi hapo tu
(iv) Nyundo/ Mjuzi/ Bingwa/ Shujaa/ Mweledi/ Stadi ninakuja misumar jihadhari alama 4 x 1 = 4
d) (i) Amekomaa zaidi anajiandaa kwa fikira na vitendo alama 2
(ii) Kuifaa nchi yake kuleta maendeleo /kurekebisha kujenga mji/ kuondoa uhasama alama 2
e. (i) Yeye hana kinyongo anapokuja (lakini kwa waliomtenda na wale wanaomngojea kwa maovu atapambana nao) alama 2
f) (i) Mwando – Mwanzo
(ii) Ningambwa – Ningeambiwa 2×1 =2
g) sifa inayopatikana katika shairi kuhusu mhusika
(i) hajabadilika (ni ile nyundo / bado yu tayari)
(ii) bado yu tayari kupambana na matatizo na anaweza/ mtekelezi 2 x 1 = 2
USHAIRI WA 2
Soma shairi hili kisha ujibu maswali.
Jukwani naingia, huku hapa pasokota,
Kwa uchungu ninalia,hii tumbo nitaikata,
Msiba mejiletea,nimekila kiso takata,
We tumbo nitakupani,uwe umetosheka?
Wazee hata vijana,wote umewasubua,
Huruma nao hauna,heshima kawakosea,
Ukambani na Sagana,hata mbwa wararua,
We tumbo nitakupani,uwe umetosheka?
Wahasibu ofisini,kibwebwe mejifunga,
Miaka mingi vitabuni,ili wasikose unga,
Nadhari wanadhamini,hesabu wanazirenga,
We tumbo nitakupani, uwe umetosheka?
Wapenzi wa kiholela,pia wanakuogopa,
Baada yao kulala, wana wao wanatupa,
Wakihitaji chakula,wanachokora mapipa,
We tumbo nitakupani,uwe umetosheka?
Wafugaji hata nao,kama dawa wakwamini,
Hawajali jiranio,wamesusia amani,
Wanaiba ng’ombe wao,na kuzua kisirani,
We tumbo nitakupani,uwe umetosheka?
Nayo mizozo ya maji, kaonekana kwa mara,
Hiyo nayo ni dibaji,sababu sio harara,
Njaa wahepe wenyeji, huo ndio mkarara,
We tumbo nitakupani,uwe umetosheka?
Ningeweza kukuuza,ingekuwa siku njema,
Tena kwa bei ya meza,sokoni nimesimama,
Wala tena singewaza,kuhusu wali na sima,
We tumbo nitakupani,uwe umetosheka?
Hatima umefikika,naenda zangu nikale,
Mate yanidondoka,kwa mnukio wa wale,
Naomba kwenda kukaa,wala sio nikalale,
We tumbo nitakupani,uwe umetosheka?
Maswali
- Lipe anwani mwafaka shairi hili. (Alama 2)
- Shairi hili ni la aina gani? Toa sababu. (Alama 2)
- Huku ukitolea mifano mwafaka, taja arudhi zilizotumiwa katika ubeti wa tatu. (Alama 4)
- Andika ubeti wa nne kwa lugha nathari. (Alama 4)
- Thibitisha kuwepo kwa idhini ya ushairi. (Alama 2)
- Taja madhila anayoelezea mtunzi wa shairi hili yaletwayo na tumbo. (Alama 4)
- Elezea maana ya maneno yafuatayo. (Alama 2)
(a) Dibaji
(b) Harara
MWONGOZO WA KUSAHIHISHA USHAIRI WA 2
1.
i) – Tumbo lisilotosheka
– Matatizo ya tumbo 2×1=2
ii) – Tarbia- mishororo minne 2×1=2
iii) – Mishororo
- Vina vya kati (ni) na vya mwisho (nga)
- Vipande viwili- utao na ukwapi
- Kibwagizo
- Mizani (urari wa mizani ukwapi 8 na utao 8) jumla 16 4×1=4
iv) – Wapendanao mapenzi yasiyo na dhati wanakuogopa. Wapatao mimba, watoto wao hawajali. Watoto watakapo chakula huwa wanatafuta mapipani. Tumbo nikupe nini ili utosheke?
4×1=4
v) – Kukosa heshima- hata mbwa wararua
– Ufisadi- hesabu wanazirenga
– Kutowajibikia wana- wanachokora mapipa
– wizi- wa ng’ombe
– Mizozo/ kutoelewana- mradi waliepe njaa 4×1=4
vi) – Dibaji- Thibitisho/ uhalali
Harara- hasira/ hamaki 2×1=2
USHAIRIWA 3
Soma shairi lifuatalo kisha ujibu maswali.
LAU HAKUNA MAUTI. Na Abdalla Said Kizere
- Lau dunia nanena, tuseme si ati ati,
Mauti kawa hakuna, katika wote wakati,
Vipi tungelisongana, tunaoishi tiati?
Lau hakuna mauti, vipi tungelisongana?
- Dunia ingetatana, na kizazi katikati,
Huku kwazaliwa bwana, kule kwazawa binti,
Vipi tungelioana, na kuzaa hatuwati?
Lau hakuna mauti, vipi tungelisongana?
- Lau mauti hakuna, tungesongana sharuti,
Kwa viumbe kukazana, wanadamu na manyati,
Vipi tungelijazana, kwa kusitawi umati?
Lau hakuna mauti, vipi tungelisongana?
- Walakini Subuhana, kapanga sisi na miti,
Ili tusizidi sana, si wengi na si katiti
Maisha ya kupishana, yule ende yule keti,
Lau hakuna mauti, vipi tungelisongana?
- Ndipo dunia kufana, ikawa kama yakuti,
Kwa uwezowe Rabana, kaipanga madhubuti,
Maisha kugawiana, kayagawa kwa mauti,
Lau hakuna mauti, vipi tungelisongana?
- Njia ingekuwa hapana, pembeni na katikati,
Sote tungeambatana, kama ukosi na shati,
Na njaa ingetutafuna, pa kulima hatupati,
Lau hakuna mauti, vipi tungelisongana?
- Peleleza utaona, hayataki utafiti,
Kama tungelikongana, ingekuwa ni bahati,
Vipi tungesukumana, katika hiyo hayati?
Lau hakuna mauti, vipi tungelisongana?
- Mbele sitokwenda tena, hapa mwisho nasukuti,
Yaoleni waungwana, shauri yake Jabaruti,
Yote tuloelezana, katenda bila senti,
Lau hakuna mauti, vipi tungelisongana?
MASWALI
a) Je, hili ni shairi la bahari gani? Eleza (alama 2)
b) Eleza vile mwandishi alivyotumia uhuru wa kishairi (alama 4)
c) Eleza umbo la shairi hili (alama 4)
d) Fafanua ujumbe unaojitokeza katika ubeti wa tano (alama 4)
e) Andika majina mawili ya Mungu kwa mujibu wa shairi (alama 2)
f) Kwa kutolea mifano, eleza mbinu mbili za lugha zilizotumiwa katika shairi hili (alama 2)
g) Eleza maana ya maneno yafuatayo kulingana na shairi (alama 2)
(i) Tiati _________________
(ii) Shani_________________
MWONGOZO WA KUSAHIHISHA USHAIRI WA 3
- (i) Tarbia – – mishororo mine
(ii) Pindu – utao katika mkarara ndio kianzio cha ubeti unaofuatia mf. Ubeti 3
iii) Mtiririko – vina vya kati vinafanana na vya mwisho pia vinafanana katika shairi lote
Vya kati vya mwisho
na, ti,
na, ti,
na, ti,
ti, na.
(iv) mathnawi – lina vipande viwili – utao na ukwapi
b) (i) Inkisari –kwazawa, ńgekuwa, ńgetutafuna, nanena, sitokwenda
- Tabdila – Sharuti badala ya sharti
- Kuboronga sarufi – mauti kawa hakuna – ikiwa hakuna mauti,
– katika wote wakati – katika wakati wote
- Lahaja (ya kimvita) – hatuwati (hatuwachi)
- – yaoleni (yaoneni)
c)
- Beti 8
- Mishororo 4 katika kila ubeti
- mizani 16 katika kila mshororo
- vina vya kati vya mwisho
na, ti,
na, ti,
na, ti,
ti, na.
- vipande viwili – utao na ukwapi
- Lina kibwagizo kinarudiwarudiwa “lau hakuna mauti, vipi tungelisongeni
d) (i) Dunia haiwezi kujaa watu kupita kiasi
(ii) Mwenyezi Mungu anajua kupanga
- Baadhi ya watu wafe na baadhi wazaliwe
- Bila kifo tungesongamana/jaa sana
e) (i) Subuhana
(ii) Rabana
(iii) Jabaruti
f) (i) Balagha – k.v Vipi tungelisongana, tunaoishi tiati?
(ii) Tashbihi – ikawa kama ya kuti
- Kama ukosi na shati
(iii) Takriri – si ati ati
- Lau hakuna mauti, vipi tungelisongana?
USHAIRI WA 4
Soma shairi lifuatalo, kisha ujibu maswali; (alama 20)
Sinisumbuwe akili, nakusihi e mwendani,
Afiya yangu dhahili, mno nataka amani,
Nawe umenikabili, nenende sipitalini,
Sisi tokea azali, twenda zetu mizimuni,
Nifwateni sipitali, na dawa ziko nyumbani?
Mababu hawakujali, wajihisipo tabani,
Tuna dawa za asili, hupati sipitalini,
Kwa nguvu za kirijali, mkuyati uamini,
Kaafuri pia kali, dawa ya ndwele Fulani,
Nifwateni sipitali, na dawa ziko nyumbani?
Mtu akiwa halali, tumbo lina walakini,
Dawa yake ni subili, au zongo huauni,
Zabadi pia sahali, kwa maradhi yalondani,
Au kwenda wasaili, wenyewe walo pangani,
Nifwateni sipitali, na dawa ziko nyumbani?
Mtu kwenda sipitali, ni kutojuwa yakini,
Dakitari k’ona mwili, tanena kensa tumboni,
Visu vitiwe makali, tayari kwa pirisheni,
Ukatwe kama figili, tumbo nyangwe na maini,
Nifwateni sipitali, na dawa ziko nyumbani?
Japo maradhi dhahili, kuteguliwa tegoni,
Yakifika sipitali, huwa hayana kifani,
Wambiwa damu kalili, ndugu msaidieni,
Watu wakitaamali, kumbe ndiyo buriani,
Nifwateni sipitali, na dawa ziko nyumbani?
Mizimu wakupa kweli, wakueleze undani,
Maradhiyo ni ajali, yataka vitu thamani,
Ulete kuku wawili, wa manjano na kijani,
Matunda pia asali, vitu vyae chanoni,
Nafwatani sipitali, na dawa zi mlangoni?
MASWALI – USHAIRI (ALAMA 20)
a) Lipe kichwa mwafaka shairi hili. (alama 2)
b) Mtunzi alikuwa na lengo gani alipotunga shairi hili? (alama 2)
c) Mbona mshairi hataki kwenda hospitali? (alama 4)
d) Kwa kuzingatia muundo wa shairi hili, eleza mbinu zilizotumika (alama 6)
e) kwa nini mshairi alitumia ritifaa katika ushairi? (alama 2)
f) Andika maana ya maneno yafuatayo yalivyotumika katika shairi (alama 4)
i) Dhahili
ii) Azali
iii) Sahali
iv) Tumbo nyangwe
MWONGOZO WA KUSAHIHISHA USHAIRI 4
a) i) Sipitali sendi/ siendi
ii) Udhaifu wa hospitali
iii) Umaarufu wa miti- shamba
b) i) Kupigia debe miti- shamba
ii) Kukosoa huduma za hospitali
c) i) Tangu zamani, wao huenda mzimuni
ii) Madawa ya asili yapo
iii) Hapendi upasuaji
- Mtu anaweza kupoteza maisha
- Tunafuata kieleleza cha mababu wetu
d) i) Inkisani- tabani, wambiwa
ii) Mazida- Afiya
- Takhmisa- Mishororo tano
- Kibwagizo- Nifwateni sipitali, na dawa ziko nyumbani?
- Mtiririko (vina vya kati ni “li” ilhali vya utao ni “ni”
- Mizani kumi na sita kwa kila mshororo
e) Inkinsani
f) i) Dhalili- Hafifu, isio na nguvu
ii) Azali- zamani
- Sahali- Nafuu
Tumbo nyangwe- Utumbo mdogo
USHAIRI WA 5
1. Soma shairi lifuatalo kwa makini kisha ujibu maswali.
Niokoa Muokozi, uniondolee mashaka.
Kuyatukua siwezi, mjayo nimedhikika
Nimekithiri simanzi, ni katika kuudhika
Mja wako nasumbuka, nipate niyatakayo.
Mja wako nasumbuka, nataka kwao afua
Nirehemu kwa haraka, nami nipate pumua
Naomba hisikitika, na mikono hiinua
Mtenda ndiwe Moliwa, nipate niyatakayo.
Mtenda ndiwe Moliwa, we ndiwe Mola wa anga
Mazito kuyaondoa, pamoja na kuyatenga
Ukauepusha ukiwa, ya pingu zilonifunga
Nikundulia muwanga, nipate niyatakayo
Muwanga nikundulia, nipate toka kizani
Na huzuni n’ondolea, itoke mwangu moyoni
Mambo mema niegheshea, maovu nisitamani.
Nitendea we Manani, nipate niyatakayo.
Igeuze yangu nia, dhaifu unipe mema
Nili katika dunia, kwa afia na uzima
Moliwa nitimizia, yatimize yawe mema
Nifurahike mtima, nipate niyatakayo.
- Shairi hili ni la bahari gani? Eleza. (alama 2)
- Taja madhumuni ya shairi hili. (alama 3)
(c) Eleza muundo wa shairi hili. (alama 4)
(d) Thibitisha namna uhuru wa kishairi unaibuka katika shairi. (alama 4)
(e) Andika ubeti wa pili katika lugha sufufu. (alama 4)
(f) Toa maana ya:
- Nimedhikika
- Muwanga nikundulia
- Nifurahike mtima (alama 3)
MWONGOZO WA KUSAHIHISHA USHAIRI WA 5
1. a) Pindu- Kifungu katika mshororo wa mwisho wa ubeti kuanza ubeti mpya 1×2=2
b) –Kuonyesha kuwa mja hana nguvu
-Amekumbwa na masaibu
-Maombi kwa mola amwokoe na ampe afya
-Mungu amtoe katika giza
-Mungu ampe maisha mema
Zozote 3×1=3 mks
c) Muundo
-Tarbia
-Vina vya kati na vya mwisho
-Mizani
-Kibwagizo
4×1=4 mks
d) Inksari-
-Mjayo; Mja waho
-Nondolea
-Zilonifunga
Mazida –Moliwa
Tabdila –Afia
Kuboronga sarufi –igeuze yangu nia
4×1=4mks
e) Kiumbe wako nimeteseka mno. Naomba unipe afueni na unirehemu. Ninaomba nikikusudia. Wewe ndiwe Muumba unayeweza kunipa niyahitajiyo. 4×1=4mks
f) i) Nimeteseka au ni taabani
ii) Nimulikie; niletee nuru, nizinduke
iii) Nichangamke au nistarehe moyoni.